Pata ujuzi, uchambuzi, habari za kiteknolojia na apps za kijanja ukiwa na smatskills, kuwa karibu ili ujifaidi mwenyewe

Breaking

30.10.17

Historia ya Jamii Forum

Historia Uanzilishi

JamboForums ilikuja baada ya kuwa na majukwaa mbalimbali kama Tanzania Economic Forum, Habari Tanzania, Jambo Network, Jambo Radio na Jambo Videos.

Kila tovuti ilikuwa na malengo tofauti lakini yote yakilenga kuwahudumia watu wa nyanja husika kuweza kupata sehemu ya kusemea au kubadilishana mawazo.

Lengo kuu la JF likiwa ni kuanzisha Jamvi moja ambapo wadau watakutana na kubadilishana mawazo huku wakikubali kutokubaliana (utofauti wa mawazo) na kujenga mijadala endelevu. Katika Jambo Network (jambonetwork.com) au JamboRadio.com mijadala ilikuwa kwa mtindo wa chat ambapo hakukuwa na kumbukumbu baada ya mjadala, hii ilipelekea mijadala mingi kuwa inarudiwa na kusababisha kukosa mwelekeo kabisa.

Katika uanzilishi lengo kubwa lilikuwa kuwafikia wazungumzaji wa kiswahili wa eneo la Maziwa Makuu na hata watumiaji wengi wa Kiingereza lakini wenye kupenda kujua habari za ukanda huu.

Mkusanyiko wa majukwaa haya ulipelekea kuwa na kusanyiko moja ambalo kwa wakati huo (2006) liliitwa JamboForums.com, jina ambalo lilitumika hadi mwezi Mei 2008


Mabadiliko ya jina
Mwaka 2008 yalifanyika maamuzi ya haraka na ya lazima kwa wakati huo kwa kubadili jina kutoka Jambo Forums kwenda JamiiForums. Jina la JamiiForums lilichagizwa na kubakia na kifupi cha JF kutoka kuwakilisha neno JamboForums na sasa kuwakilisha neno JamiiForums.

Jina lililazimika kubadilishwa kutokana na mgongano wa matumizi ya jina la JamboForums ambapo lilikuwa halijachukuliwa haki miliki (copyrights) za jina ingawa baadaye walifanikiwa kulimiliki kihalali.

Uongozi haukutaka kusimamisha moja kwa moja matumizi ya JF hivyo wakafikiria jina mbadala la JamboForums na kubaini kuwa tayari hili kusanyiko la wadau ni kusanyiko la Jamii, na bado Jamii ilikuwa ikiendelea kutunza JF kama wengi wanavyopenda kufupisha.

Madhumuni ya kuanzisha JF
Lengo kubwa la uanzishwaji wa JF likiwa ni kuwafikia wazungumzaji wa Kiswahili wa eneo la Maziwa Makuu na hata watumiaji wengi wa Kiingereza lakini wenye kupenda kujua habari za ukanda huu kwa kutoa uwanja huru wa kujadili kwa wanachama wake ambao sio shuruti kutumia majina yao halisi.

Maboresho 2014
Mwaka 2014 JamiiForums ilifanya mchakato wa mabadiliko kwa msaada wa karibu wa TMF(Tanzania Media Fund). Kampuni ya Jamii Media ikiwa na tanzu mbili za JamiiForums na Fikraperu. Mabadiliko haya yaliongozwa na Maxence Melo, Mike Mushi, Mbaraka Islam, Asha Abinallah na wengineo. Mwaka tajwa mambo mengi yalirasimishwa na mpango wa JamiiForums kujiendesha ulianza kufanikiwa.


Mafanikio
Kwa miaka yote iliyodumu, Jamiiforums imekuwa msaada katika nyanja nyingi ikiwemo siasa, michezo, afya, habari na hasa habari mtambuka. Mtandao wa JamiiForums unatoa fursa ya kipekee ya kujadili habari na hoja mbalimbali badala ya habari kulishwa kwa upande mmoja.

JamiiForums imetoa fursa kwa wananchi wa kawaida kujadiliana na viongozi wa juu katika serikali na taasisi mbalimbali pia watu maarufu katika jamii ambao kwa namna moja au nyingine ingekuwa ngumu kwao kuwapata. Mfano watu maarufu ni mwanasiasa mkongwe wa Tanzania ambae alipata kuwa katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani Tanzania na kuwania urais mwaka 2010, Dr. Willbrod Peter Slaa na pia baadhi ya taasisi kubwa nchini kama TCRA ambao ni wadhibiti wa mawasiliano Tanzania.

Jamiiforums kutokana kuwa na wanachama wa aina mbalimbali ina wataalam waliobobea katika fani mbalimbali ambao wanaweza kutoa majibu ya kitaalamu kulingana na fani zao ambapo si ajabu muhusika angelipia kama wangekutana ofisini ama kuibiwa. Mifano inajumuisha ujenzi, afya, teknologia pia inajumuisha uchambuzi makini katika siasa na chaguzi za miaka nenda rudi kwa kutoa mawazo mbadala na kufikisha sauti za watu wasioweza kusikia.

Chanzo/uthibitishaji habari Jamiiforums

Hili kwa muda mrefu limekuwa swali kwa watu wengi kwa jinsi gani JamiiForums wanadhibiti habari za uongo na nini chanzo cha habari zao. JamiiForums ni mtandao wa kijamii na si gazeti wala redio lakini utofauti wake wenyewe wameweka wahariri ambao kazi yao kubwa ni kusimamia sheria za majadiliano walizojiwekea lakini pia ikiwekwa habari na wanachama wake inayotiliwa shaka basi hufatilia na kuthibisha au kubatilisha.


Fikrapevu
Kuongeza ufanisi na uhakika wa habari zake, kilianzishwa kitengo maalum kinachohusika na habari ambapo huhaririwa na waandishi na kuchapishwa kwenye mtandao wa fikrapevu.com ambapo ni gazeti mahsusi la mtandaoni kwani kuwazuia watu kuweka habari mpaka uthibitisho kwenye JamiiForums ilionekana ni ukirikitimba na ungeelekea kwenye mkwamo. Wanachama wa JF wamekuwa waungwana na pale ambapo mwanachama mwenzao akipotosha basi kuna nafasi ya kuripoti ili usawa uwekwe.

JamiiForums na chaguzi Tanzania

JamiiForums na ufisadi


Takwimu
Kwa mwaka 2012 JamiiForums ilikuwa na wanachama zaidi ya 100,000 na kupata watembeleaji 50,000 kila siku. Kulingana na mtandao wa statscrop.com ambao hupima tovuti mbalimbali, JamiiForums ina thamani ya $3,182,721.

Kufikia mwanzoni mwa mwaka 2016 JamiiForums ilifikisha wanachama Zaidi ya 320,000. Mijadala Zaidi ya laki nane na michango Zaidi milioni 15. Kwa upande wa watembeleaji…….

Wanachama wakongwe

Pamoja na JF kuwa na wanachama wengi lakini wapo wanachama walioanza tangu JamboForums inaanza mwaka 2006 na wangine wamekuwa nayo kwa takriban miaka kumi sasa. Mafano wa wanachama hao ni Mzee Mwanakijiji, Rev. Kishoka, Augustine Moshi, Kyoma, Mwawado, Mkandara, Kibunango, Steve Dii Mwafrika wa Kike, Kichuguu Choveki Masatu Masanja Quemu Mlalahoi Mtanzania Bibi Ntilie Game Theory jmushi1 Zakumi Moelex23 na wengineo wengi.


Jamiiforums kwenye mitandao ya kijamii
Pamoja na kuwa mtandao wa kijamii maarufu zaidi ukanda wa Afrika Mashariki wenye asili ya Tanzania, JamiiForums inazo kurasa kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook ikiwa na wafuatiliaji wengi zaidi Afrika Mashariki takribani 1,100,000 mpaka September 2015 pia Jamiiforums ina kurasa yake katika mtandao wa Twitter na instagram.
             Chanzo ni Plata O Plomo pamoja na Wikipedia.